UTAKATIFU NI PAMOJA NA KUSALI, KUSIFU NA KUABUDU
SURA
YA KWANZA
TUSALI KWANZA SALA YA
ASUBUHI
Kama umeanza kusoma asubuhi Sali kwanza sala hii.
+Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho
Mtakatifu. Amina.
Tuusifu Utatu Mtakatifu wa Mungu mmoja, sasa
na siku zote na milele amina. Ee utatu Mtakatifu wa Mwenyezi Mungu; +Baba,
+Mwana na +Roho Mtakatifu. Ninasadiki kuwa upo hapa na mahali pote.
Ee Mungu wangu, umeniumba, umenikomboa,
umenifanya mkristu, umenizidishia neema zako, umenitayarishia makao yangu
mbinguni.
Ee Mungu wangu, nakuabudu, nakushukuru,
nakuomba toba, nakupenda. Ee Mungu wangu, ninakutolea roho yangu, na mawazo, na
maneno, na kazi na furaha, na mateso yangu, uyapokee unipe neema yako nisitende
leo dhambi, Amina.
______________________
Ee Baba yetu Mungu mkuu,
Umenilinda usiku huu.
Nakushukuru kwa moyo,
Ee Baba, Mwana na Roho.
Nilinde tena siku hii,
Niache dhambi, nikutii.
Naomba sana Baba wee,
Baraka zako nipokee.
Bikira safi, Ee Maria
Nisipotee nisimamie.
Mlinzi mkuu malaika wee,
Kwa Mungu wetu niombee
Nitake nitende mema tu,
Na mwisho nije kwako juu. Amina.
NIA NJEMA.
Kumheshimu Mungu wangu
Namtolea roho yangu,
Nifanye kazi nipumzike
Amri zake tu nishike
Wazo, neno, tendo lote
Namtolea Mungu pote
Roho, mwili chote changu,
Pendo na uzima wangu
Mungu wangu nitampenda,
Wala dhambi sitatenda.
Jina lako nasifia,
Utakalo hutimia.
Kwa utii navumilia
Teso na matata pia.
Nipe, Bwana, neema zako
Niongeze sifa yako. Amina.
SALA YA MATOLEO.
Ee Yesu, kwa mikono ya Bikira Maria, na kwa
maungano na sadaka yako kuu, ninakutolea sala, matendo, masumbuko na furaha
zangu zote za leo. Ee Yesu, ufalme wako utufikie.
BABA YETU.
Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku. Utusamehe
makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika
kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALAMU MARIA.
Salamu, Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe.
Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa.
Maria Mtakatifu mama wa Mungu, utuombee sisi
wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
KANUNI YA IMANI.
Nasadiki kwa Mungu Baba mwenyezi. Muumba wa
Mbingu na dunia. Na kwa Yesu Kristo Mwanae wa pekee, Bwana wetu. Aliyetungwa
kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria. Akateswa kwa mamlaka ya
Ponsiyo Pilato. Akasulibiwa, akafa, akazikwa, akashukia kuzimu. Siku ya tatu
akafufuka katika wafu. Akapaa mbinguni, amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi.
Toka huko atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu.
Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, kanisa takatifu
katoliki, ushirika wa watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili na
uzima wa milele ijayo. Amina.
AMRI ZA MUNGU.
1. Ndimi Bwana Mungu wako, usiabudu Miungu
wengine.
2. Usilitaje bure jina la Mungu wako.
3. Shika kitakatifu siku ya Mungu.
4. Waheshimu Baba na Mama upate miaka mingi na
heri duniani.
5. Usiue.
6. Usizini.
7. Usiibe.
8. Usiseme uongo.
9. Usitamani mwanamke asiye mke wako.
10. Usitamani mali ya mtu mwingine.
AMRI ZA KANISA.
1. Hudhuria misa takatifu, dominika na sikukuu
zilizoamriwa.
2. Funga siku ya jumatano ya majivu; usile
nyama siku ya ijumaa kuu.
3. Ungama dhambi zako walau mara moja kila
mwaka.
4. Pokea Ekaristi takatifu hasa wakati wa
Paska.
5. Saidia kanisa katoliki kwa zaka.
6. Shika sheria katoliki za ndoa.
Ee Maria Bikira Mtakatifu, Mama wa Mungu na
Mama yangu, nawe Mtakatifu Yosefu, Nawe malaika mlinzi wangu, nanyi watakatifu
somo wangu, nanyi watakatifu wote, niombeeni nipate kuacha dhambi, nilindeni
siku ya leo na siku zote, na saa ya kufa kwangu, Amina.
SALA YA IMANI.
Mungu wangu, nasadiki maneno yote.
Linayosadiki na linayofundisha Kanisa Katoliki la Roma. Kwani ndiwe
uliyetufumbulia hayo. Wala hudanganyiki, wala hudanganyi. Amina.
SALA YA MATUMAINI.
Mungu wangu, natumaini kwako, nitapewa kwa
njia ya Yesu Kristo. Neema zako hapa duniani, na utukufu mbinguni. Kwani ndiwe
uliye agana hayo nasi, nawe mwamini. Amina.
SALA YA MAPENDO.
Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote. Kwani
ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu, kama nafsi
yangu, kwa ajili yako. Amina.
SALA YA KUTUBU.
Mungu wangu nimetubu sana, niliyokosa kwako.
Kwani ndiwe mwema, ndiwe nwenye kupendeza. Wachukizwa na dhambi, basi sitaki
kukosa tena. Nitafanya kitubio, naomba neema yako, nipate kurudi. Amina.
SALA KWA MALAIKA MLINZI.
Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari
zote, za roho na za mwili. Amina.
MALKIA WA MBINGU
Malkia wa mbingu, furahi Aleluya,
Kwani uliyestahili kumchukua Aleluya,
Amefufuka alivyosema Aleluya
Utuombee kwa Mungu Aleluya
Furahi, shangilia, Ee Bikira Maria Aleluya,
Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.
Tuombe:
Ee Mungu uliyependa kuifurahisha dunia kwa
kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao; fanyiza twakuomba, kwa ajili ya
Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya
Kristu Bwana wetu. Amina.
Atukuzwe Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu,
nikama mwanzo, sasa na siku zote na milele Amina.
Roho za waumini marehemu wapate rehema kwa
Mungu wapumzike kwa amani.
Mt. Marko Mwinjili utuombee.
Kwa jina la +Baba na la +Mwana na la +Roho
Mtakatifu. Amina
SALA KABLA YA KUPOKEA
EKARISTI TAKATIFU.
IMANI
Kristu Yesu Mwokozi
wangu, nasadiki upo kweli katika altare hapa. Nasadiki kwamba nitapewa sasa
hivi mwili wako na damu yako pamoja na roho yako na umungu wako. Nasadiki kwani
ndiwe mwenyewe
uliyetueleza.
MATUMAINI
Ee Mungu wangu umesema
kwamba, watu waliokutumainia hawatadanganyika kwako. Basi nimekutumainia kwamba
utatimiza maagano uliyoagana nasi, kuwa nikilishwa mwili wako duniani hapa,
nitapata kufika kwako mbinguni na
kukuona milele.
KUABUDU
Yesu mwema, nakuabudu
katika hostia takatifu; nakuungama ndiwe Muumba wangu na Bwana
wangu;nakunyenyekea; nakutolea heshima na chochote changu.
KUTUBU
Bwana wangu, sistahili
uingie kwangu, kwani mkosefu mimi, nikatenda dhambi nyingi; nawe ndiwe mwenye
utakatifu kamili, wapenda utakatiu, wachukia maovu yangu. Una enzi kuu, waweza
kufuta dhambi zangu kabisa. Basi nazichukia nami, nakuomba uniondolee,
unitakase kabisa,
nipate kukupokea kwa moyo mwema.
MAPENDO
Ee Mungu, umejifumba
katika sakramenti ya ekaristi kwa sababu umenipenda mno! Unitie moyo wa kukupenda
sana, vilevile ulivyonipenda.
UNYENYEKEVU
Ee Yesu wangu, Bwana
wangu, una utakatifu kamili; nami si mtakatifu kabisa, ila ni mtenda dhambi
nyingi. Sistahili kweli unijie kwangu: useme neno tuu na roho yangu ipone.
KUTAMANI
Roho yangu inakutamani
Mungu wangu, ndiwe mwenye kunifurahisha; ndiwe mwenye kuniletea heri. Unionee
huruma, unifanyie neema kuu, uje kuniangalia, uje kukaa kwangu, nami nikae
nawe. Amina.

Maoni
Chapisha Maoni
thank you very much asante sana